![Bw Kabila Kinshasa 9 Desemba, 2018](https://ichef.bbci.co.uk/news/660/cpsprodpb/1DBB/production/_104711670_kabila.jpg)
Bw Kabila anasema bado safari ni ndefu
Rais wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila amesema ataendelea kushiriki katika
siasa nchini humo hata baada ya kuondoka madarakani baada ya uchaguzi
utakaofanyika wiki mbili zijazo.
Aidha, hajafutilia mbali uwezekano wake wa kuwania tena urais uchaguzi mkuu mwingine utakapoandaliwa mwaka 2023.Bw Kabila alitarajiwa kuondoka madarakani miaka miwili iliyopita baada ya kuongoza kwa mihula miwili kwa mujibu wa katiba.
Hata hivyo, uchaguzi mkuu nchini humo uliahirishwa mara kadha, serikali ikisema maandalizi yake hayakuwa yamekamilika vyema.
Upinzani ulitazama hilo kama njama ya Bw Kabila kutaka kuendelea kuongoza.
Mwezi Agosti, Bw Kabila alimtangaza mshirika wake wa karibu Emmanuel Ramazani Shadary ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya ndani kuwa mgombea wa muungano wa kisiasa unaotawala kwa sasa.
Bw Shadary amewekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya kutokana na tuhuma za ukiukaji wa haki za kibinadamu.
Katibu wa chama cha upinzani cha Movement for the Liberation of Congo (MLC), Eve Bazaiba, ameambia BBC kwamba Bw Shadary atadhibitiwa na Bw Kabila na kwamba kimsingi itakuwa ndiye anayeongoza nchi.
"Anataka tu kusalia madarakani. Hata kama alimchangua Shadary, Shadary ni mtu tu wa kuonekana, ndiye atakayemuongoza Shadary kwa kila jambo. Kiuhalisia, atakuwa bado ndiye rais."
Bi Bazaida amesema serikali imekuwa ikiwazuia wanasiasa wa chama cha MLC kufanya kampeni.
![Emmanuel Ramazani Shadary](https://ichef.bbci.co.uk/news/624/cpsprodpb/34D9/production/_102892531_3fce1e93-e24e-4f0c-b014-f9a4f337c333.jpg)
Kwenye mahojiano na shirika la habari la Reuters, Rais Kabila amesema: "Mbona tusisubiri hadi mwaka 2023 … ndipo tuwe na uwazi kuhusu mambo haya," alisema.
"Maishani sawa na ilivyo katika siasa, hauwezi kufutilia mbali jambo kabisa."
Kumekuwa na wasiwasi kutoka kwa upinzani na jamii ya kimataifa kuhusu iwapo uchaguzi wa DRC utakuwa huru na wa haki.
Lakini Bw Kabila amesema wasiwasi huo haufai kuwepo.
![Martin Fayulu Novemba 11, 2018 Geneva](https://ichef.bbci.co.uk/news/624/cpsprodpb/1298/production/_104506740_gettyimages-1060576682.jpg)
Martin Fayulu awali alitangazwa kuwa mgombea wa muungano wa upinzani
"Tunakusudia kadiri ya uwezo wetu kuhakikisha uchaguzi huu hauna kasoro hata moja. Waangalizi wanaofikiria kwamba uchaguzi huu hautakuwa huru na wa haki, bado sijawaona wakija hapa na kusema ni kitu gani tumekikosa."
Kabila aliingia madarakani akiwa na miaka 29 baada ya babake Laurent Desire Kabila kuuawa na mlinzi wake mwaka 2001.
Aliahidi kurejesha amani na kuangamiza ufisadi na amekuwa akitaja hayo kama baadhi ya mafanikio ya utawala wake.
DRC ilikuwa imekabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1998 na mwaka 2003 ambapo takriban watu 5 milioni walifariki kutokana na vita, njaa na maradhi.
"Tuna majuto yoyote? La hasha, hata kidogo. Tumepata mafanikio mengi. Jambo kuu zaidi ni kwamba tuliweza…kuliunganisha tena taifa na kulirejesha kwenye mkondo ufaao."
Kabila amesema anataka kusalia katika siasa ili kulinda mafanikio hayo na kuongeza kwamba wanaotaka kutoa uamuzi kuhusu mafanikio yake wanaweza kusubiri hadi amalize kazi yake.
"Bado kuna safari ndefu sana mbele yetu na kuna sura nyingi sana ambazo zitaandikwa kabla tuanze kuandika vitabu vya historia."
![Vital Kamerhe (kushoto) na Felix Tshisekedi](https://ichef.bbci.co.uk/news/624/cpsprodpb/8A70/production/_104504453_tshisekedi.jpg)
Felix Tshisekedi ameungana na Vital Kamerhe ambaye ni mgombea mwenza wake
Katiba nchini DRC inamzuia mtu aliyeongoza kwa mihula miwili mfululizo kuwania tena urais, lakini haijazuia mtu kama huyo kuwania tena baada ya kiongozi mwingine kuingia madarakani.
Baadhi wanasema huenda kikawa kisa kama cha rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye baada ya kuongoza kama rais kati ya 2000 na 2008, alikuwa waziri mkuu kati ya 2008 na 2012 kabla ya kurejea tena kama rais wa nchi hiyo. Alibadilishana na mwandani wake Dmitry Medvedev ambaye kwa sasa ndiye waziri mkuu.
Comments
Post a Comment
Here