Baraza la Sanaa la Taifa nchini Tanzania (BASATA) limetetea hatua yake ya kuwapiga marufuku wanamuziki Diamond Platnumz na Rayvanny dhidi ya kufanya tamasha zozote kwa muda usiojulikana.
Basata walitangaza uamuzi huo Jumanne wakisema hatua yao ilitokana na wawili hao kutofuata maagizo waliyopewa na baraza hilo wimbo wao wa Mwanza ulipopigwa marufuku Novemba.
Wasanii hao wawili walikuwa awali wametakiwa kuuondoa wimbo wao kwa jina 'Mwanza' kutoka kwenye mitandao ya kijamii, lakini wimbo huo umeendelea kuwepo kwenye YouTube na wamekuwa wakiucheza kwenye tamasha mbalimbali.
Kadhalika, Diamond ambaye jina lake halisi ni Nasibu Abdul Juma Issaack, Rayvanny ambaye jina lake halisi ni Raymond Shaban Mwakyusa na Wasafi Limited walikuwa wametakiwa kila mmoja kulipa faini ya shilingi milioni tatu za Tanzania kabla ya siku 14 kupita
"Baraza limefikia maamuzi ya kuwafungia rasmi kutokana na wasanii hawa kuendelea kuonyesha dharau na utovu wa nidhamu kwa mamlaka zinazosimamia masuala ya sanaa nchini na uvunjifu wa maadili uliokithiri," Basata walisema Jumanne kupitia taarifa.
Diamond Platnumz na kikosi chake cha Wasafi wameandaa tamasha kadha huu wa Krismasi, ambapo walitarajiwa kutumbuiza mjini Embu katika eneo la Mlima Kenya nchini Kenya tarehe 24 Desemba, na mkesha wa Mwaka Mpya amepangiwa kuwa bustani ya Uhuru, Nairobi.
Basata wanaweza kumzuia Diamond kutoka nje ya Tanzania?
Bi Agnes Kimwaga ambaye ni afisa habari mkuu wa Basata, amemwambia mwandishi wa BBC Maximiliana Mtenga kwamba baraza hilo lina mamlaka ya kumzuia msanii kutoka nje ya Tanzania.
"Kwa mujibu wa kanuni za Basata ya 2018, baraza linawajibika kumpa kibali msanii yeyote anapotoka nje ya nchi kwenda kufanya shughuli za sanaa. Kwa hivyo sisi ndio tutakaokutambulisha, na kibali hicho kitakuruhusu kuweza kutoka uwanja wa ndege kwenda kufanya shughuli yoyote ya sanaa nje ya nchi.
"Ikiwa tumekufungia kwa mujibu wa sheria, nani atakupatia kibali cha kukutambulisha kutoka nje ya mipaka ya nchi kwenda kufanya shughuli za sanaa.
"Kwa mujibu wa sheria tunaweza kumzuia kwenda kufanya nje ya nchi kwa sababu tutakataa kutoa vibali vya kumruhusu kutoka."
Bi Kimwaga amesema sababu ya kumfungia kwa muda usiojulikana ni kwa sababu inategemea kasi ya wahusika kutekeleza masharti waliyowekewa.
Miongoni mwa masharti hayo ni kulipa faini na kuuondoa wimbo huo kutoka kwenye mitandao ya kijamii.
Basata amesema kwa sasa bado ni mapema kuzungumzia uwezekano wa wanamuziki hao kupelekwa mahakamani iwapo wataendelea kukaidi maagizo ya baraza hilo.
"Itakuwa ni haraka sana kusema kwamba tunampeleka mahakamani. Basata ni walezi wa wasanii, na nina uhakika kama walezi mzazi yeyote mtoto anapokosea unajitahidi kwanza wewe kama mzazi kwa nafasi yako kujaribu kumrekebisha na kuhakikisha anafuata yale anayoyafanya. Tulikuwa na uhakika atafuata masharti."
Hatua ya Basata kuwafungia wanamuziki hao imezua mjadala mkali mitandao ya kijamii na pia kuzua utata kuhusu tamasha ambazo Rayvanny na Diamond na kampuni ya Wasafi walikuwa wanayaandaa hasa katika nchi jirani ya Kenya.
Mvutano miongoni mwa Watanzania
Watanzania wamekuwa wakitoa maoni mbalimbali kuhusu hatua hiyo ya Basata mtandaoni.
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Bi Fatuma Karume amekosoa uamuzi wa Basata na kusema wamekiuka katiba katika kufanya hivyo.
"Wanamuziki wamekua watoto wa Basata. Can you imagine mtu anachukua haki ya mwenzake ya kikatiba ya kufanya Kazi kwa sababu kamdharau? 🤣🤣 Sasa watoto wake atalishwa na Basata? Maana maashallah Diamond si mvivu wakufanya Kazi na kazaa kama alivyoelekezwa na Magu."
"Hili sakata la Basata: sheria yetu inasema "audi alteram partem" sikiliza upande wa pili kabla ya kutoa uamuzi. Hao Basata walimuita 💎 wakimpa muda wakujieleza kabla hawajatoa maaumuzi? Walimpa notice ya kutosha ajekujieleza? Nchi inaendeshwa kama kijiji cha Chief Mapepe!"
Lakini Nyamria Kikube Kigeso anaiunga mkono Basata, anasema: "Mtu anaimba vitu vya ajabu, ameishaonywa bado anaendelea, acheni bana, katika [hili] naunga mkono, basata wako sahihi."
Basata wangembana Magufuli angekuwa mwanamuziki?
Miongoni mwa wanaotofautiana na Basata ni Mbunge wa Arusha Godbless Lema ambaye anaamini Diamond na Rayvanny hawakufaa kufungiwa kamwe.
Amerejelea kisa cha Naibu Spika Dkt Tulia Ackson Mwansasu kuonekana kwenye video akiuimba na kucheza wimbo Mwanza akiwa nchini Burundi, wiki chache zilizopita, kipindi ambacho alikuwa amemuomba Spika wa Bunge Ndugai aitishe kamati ya maadili ya Bunge juu ya kitendo cha naibu spika huyo.
Baada ya kufungiwa kwa Diamond na Rayvanny Jumanne, aliandika kwenye Twitter: "Tofauti na muziki kuwa burudani muziki pia ni biashara na uchumi, mwanamuziki Diamond na Rayvany wamefungiwa na BASATA kufanya kazi ya muziki ndani na nje ya nchi.
"Nafikiri Diamond akuona kosa la nyimbo yake baada ya kuona Mh NS Tulia akionekana kufurahia muziki huo nchini Burundi."
Leo ameongeza kwamba vigezo sawa vingetumiwa, basi hata tamko la Rais Magufuli lingefungiwa na Basata.
"Maneno haya aliyo ongea Rais Magufuli yangelikuwa ni muziki bila shaka Basata wangeufungia muziki huu haraka sana," ameandika.
Baadhi ya wachangiaji mitandaoni, wamekosoa pia hatua ya Basata na kusema wangefungia hata Bob Marley.
Richard Mabala anayejiita pia MabalaMakengeza ameandika kwenye Twitter: "Naomba BASATA wapige marufuku nyimbo za Bob Marley (Mallya) maana ni mchochezi. Get up stand up, stand up for your rights ... dah! Hatareeeee."
Allan Lucky anayejiita A.K.A Google amekuwa akiyacheka yaliyojiri jana, ambapo Mourinho pia alifutwa kazi Manchester United, na upinzani ukawa na tamko Zanzibar.
"Huku tamko la vyama vya siasa, kule Mourinho, hapa kati Diamond na BASATA, pembeni kidogo FA na uturi, kando yake hapo kuna Vee Money na tuviatu. Mambo ni [moto]."
Lord_And_Master, anakosoa pande zote mbili: "Kwa kweli Basata wanazingua sana hawajui jinsi gani watu wanvyo hustle kutoka kimaisha hawana mchango wowote na wasanii Lakini pia acha Diamond anyooshwe na hiyohiyo serikali anayo isifia na kuiimba kuwa inafanya kazi. Na badoooo."
@arnoldomutiti, anasema yeye angelikuwa Diamond, angefika Kenya liwe liwalo.
"Mimi kama ni diamond napanda modern coast anakuja nayo Kenya. Naonyesha basata kweli nobody can stop reggae," anasema.
Diamond, Rayvanny na Wasafi wamesemaje?
Wawili hao kufikia sasa hawajatoa tamko lolote rasmi kuhusu hatua hiyo ya Basata.
Lakini Jumanne, taarifa zake kufungiwa zikisambaa, amepakia picha mbili kwenye Instagram akionekana kucheka na kufurahia sana akiwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambapo kwenye kitambulisha mada amemwita 'Kipenzi Chetu'.
Baada ya meneja wa Manchester United Jose Mourinho kufutwa kazi, kiungo wa kati wa Ufaransa Paula Pogba alipakia picha mtandaoni, akiwa ametoa jicho na tabasamu, na kwenye maelezo 'Caption This', kwa maana ya weka maelezo kwenye picha.
Diamond, aliandika maelezo 'Please Caption this....... mie naanza na hizi mbili...1. "Basi mie na @rayvanny Tukatumbukia Pale Stejini" "Eti @_esmaplatnumz anamwita TARZAN kwasababu ya Vitopu vyake"😂 Earlier Today with our #FormerPresident #Daddy #KipenziChetu #BongoflevaGodFather Hon: @jakayakikwete."
Diamond Platnumz alipozuiwa uwanja wa ndege Dar
Julai mwaka huu, mwanamuziki huyo alizuiwa kwa muda uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam kutokana na kutokuwa na kibali kutoka kwa Basata.
Basata walijitetea kwa kuandika: "Utaratibu wa msanii kuwa na kibali anapoenda nje, yaani kutambua wapi anaelekea kikazi si mpya.Upo ktk kanuni toka awali. Lengo ni kumhakikisha ulinzi wa haki na usalama wake pale kutakapotokea suala lisilo rafiki. Pia,kumuaga kwa kukabidhi bendera na mapokezi ikibidi."
Walikuwa wakiujibu ujumbe kwenye ukurasa wao wa Twitter wa Jamii Forums waliokuwa wameandika: "Julai, 26 BASATA ilimzuia Msanii Diamond kwenda kufanya 'show' nje ya nchi akiwa katika uwanja wa JKNIA kwa kukosa kibali kutoka BASATA."
Mwezi Agosti, taarifa zilisambaa mtandaoni kwamba Diamond alikuwa amezuiwa kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya sherehe ya siku ya kuzaliwa kwa mwanawe.
Basata walikanusha taarifa hizo na kusema ni za uzushi. Walisema: "Taarifa inayosambaa kwamba Msanii Diamond anatakiwa kuchukua kibali kwenda kuhudhuria sherehe ya kuzaliwa mwanaye si ya kweli.Vibali vya kwenda nje havihusiani na safari binafsi.Tunawakumbusha wasanii kufuata taratibu zote wanapoenda kufanya maonesho nje ya nchi."
Comments
Post a Comment
Here