Waendesha mashtaka nchini Afrika
Kusini wametoa waranti ya kukamatwa kwa mke wa Rais wa zamani wa
Zimbabwe,Grace Mugabe, kutokana na tuhuma za kumshambulia mwanamitindo
mwaka 2017, Polisi wameeleza.
Hatua hiyo imekuja baada ya mahakama kuibatilisha kinga yake ya kidiplomasia mwezi Julai.Serikali ya Afrika Kusini ilikosolewa kwa kuruhusu Bibi Mugabe kuondoka nchini humo baada ya mashambulizi.
Gabriella Engels alimshutumu kwa kumpiga katika chumba cha hoteli mjini Johannesburg.
Msemaji wa polisi,Vishnu Naidoo amesema ''Siwezi kuthibitisha kuwa hati ya kumkamata Grace Mugabe ilitolewa Alhamisi iliyopita''.
Alisema polisi wanatafuta usaidizi kutoka idara ya Interpol kufanyia kazi waranti hiyo.
Haijafahamika kwa nini ripoti kuhusu waranti hiyo ilicheleweshwa na hakuna tamko lolote lililotolewa na Bibi Mugabe au mamlaka za Zimbabwe.
Familia ya Mugabe inamiliki mali nchini Afrika Kusini
Tukio la mashambulizi dhidi ya mwanamitindo lilitokea miezi mitatu kabla jeshi halijachukua mamlaka nchini Zimbabwe, hatua iliyomfanya Mugabe kujiuzulu baada ya kuwa madarakani kwa miaka 37.
Kilichotokea Johannesburg
Shambulio linaelezwa kutokea mwezi Agosti mwaka 2017 baada ya Bibi Mugabe kumkuta bi Engels akiwa na wanae wa kiume wawili, Robert na Chatunga katika chumba cha hoteli .
Wakati huo Bibi Mugabe alikuwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu ya enka yake, vyombo vya habari vya Zimbabwe viliripoti.
Engels aliweka picha mtandaoni akionyesha jeraha la kichwani. ''Wakati Grace alipoingia hakujua yeye ni nani,'' alikiambia kituo cha News 24 cha Afrika Kusini.
''Aliingia na waya wa umeme na kuanza kunipiga nao, tena na tena.Sikujua kinachoendelea.Nilihitaji kutambaa kutoka nje kabla ya kukimbia.''
Aliongeza:''Kulikua na damu kila mahali.Mikononi, kichwani, kila mahali.''
Idara ya Polisi Afrika Kusini ilifanyia uchunguzi madai hayo lakini waziri wa mambo ya nje wakati huo, Maite, Nkoana-Mashabane, alimpa kinga ya kidiplomasia bibi Grace, kumruhusu kuondoka nchini humo bila kujibu maswali yeyote.Kinga ambayo ilibatilishwa mwezi Julai.
Comments
Post a Comment
Here