Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amesema kuna mzozo wa wazi kati ya taifa lake na taifa jirani na Rwanda katika kinachoonekana kuwa kudorora zaidi kwa uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.
Rwanda na Burundi zimekuwa na uhasama kwa muda sasa, Burundi ikiituhumu Rwanda kwa kuhusika katika jaribio la kupindua serikali mwaka 2015 ambalo lilifeli.
Burundi hudai kwamba Rwanda iliwafadhili waliohusika na kwamba inatoa hifadhi kwao. Rwanda mara kwa mara imekuwa ikikanusha tuhuma hizo.
Rais Nkurunziza amemwandikia barua mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Yoweri Museveni ambaye ni rais wa Uganda akisema Rwanda sasa si mshirika tena ndani ya jumuiya bali ni kama adui.
"Rwanda ndiyo nchi pekee katika kanda hii ambayo ndiyo moja wa wahusika wakuu katika kuvuruga uthabiti wa taifa langu na kwa hivyo siichukulii kama taifa mshirika, lakini kama adui ya nchi yangu," barua hiyo, ambayo inaonesha ilitiwa saini na Bw Nkurunziza tarehe 4 Desemba, imesema.
Kiongozi huyo anataka kufanyike mkutano maalum wa EAC wa kujadili mzozo huo kati ya Rwanda na Burundi.
Viongozi wa mataifa ya jumuiya hiyo ambayo kwa sasa inajumuisha Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya, Tanzania na Sudan Kusini wamepangiwa kukutana tena 27 Desemba.
Hii ni baada ya mkutano wao wa karibuni zaidi kukosa kuendelea jijini Arusha kutokana na kutokuwepo kwa ujumbe kutoka Burundi.
Burundi inasisitiza kwamba Rwanda ndiyo chanzo kikuu cha machafuko yaliyotokea Burundi tangu Aprili 2015, na kwamba mzozo huo ulianza mapema mwaka 2010 baadhi ya makundi ya upinzani yalipoanza kusema kwamba hakungekuwa na uchaguzi 2015.
Burundi inadai kwamba Rwanda imekuwa ikihusisha katika visa vya utovu wa amani Rwanda, ikishirikiana na mkoloni wa zamani Ubelgiji.
"Rwanda ilikataa kushirikiana na kundi la pamoja la kutathmini hali halisi lakini Burundi ilishirikiana kikamilifu, na huu ni ushahidi tosha kwamba taifa hilo halijawahi kutaka ukweli ufahamuke kwa sababu ya uchokozi wake dhidi ya Burundi.
"Ni wazi kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki haifai kufumbia macho mateso haya yanayowakuta wana wa Burundi."
Burundi imesema kamwe haitakubali pendekezo la jumuiya ya kimataifa la kuruhusu vikosi kutoka nje kudumisha amani Burundi na kutolewa kwa msamaha kwa wanaodaiwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi ya serikali ya mwaka 2015 kama masharti kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa mwaka 2020.
Barua hiyo inasema kukubaliwa kwa mapendekezo hayo kutakuwa ni ukiukaji wa sheria za Burundi.
"Wahusika katika mapinduzi ya serikali kote huwajibishwa na kushtakiwa katika mahakama na majopo ya mahakama, kwa nini basi hawa wa Burundi iwe tofauti kwao?," barua hiyo inasema.
"Nasikitika, Mheshimiwa Rais (Bw Museveni) kukufahamisha kwamba kamwe sitaketi meza moja na wahusika wa mapinduzi…ninapendekeza kuandaliwa kwa kikao maalum cha viongozi wa mataifa ambacho ajenda yake itakuwa kutatua suala la mzozo wa wazi kati ya Burundi na Rwanda," amesema Bw Nkurunziza kwenye barua hiyo.
GUYS lets pray for the RWANDESE
ReplyDelete