Mbwana Ally Samatta: Nyota wa Tanzania amfunga kipa wa Liverpool aliyekumbwa na mkosi Europa League Besiktas v KRC Genk
Nahodha wa timu ya taifa ya
Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta aliendelea kutikisa ligi
ndogo ya klabu Ulaya, Europa League, kwa kufungia klabu yake mabao
mawili katika mechi iliyochezwa Alhamisi.
Aliisaidia klabu yake ya KRC Genk kuwalaza Besiktas wa Uturuki kwa mabao 4-2.Katika mechi hiyo, langoni alikuwa kipa wa Liverool Loris Karius ambaye anakumbukwa kwa kufanya makosa makubwa na kuchangia Liverpool kushindwa kwenye fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mwezi Mei mwaka huu.
Samatta alifunga bao la kwanza dakika ya 23 na kisha akaongeza la pili dakika ya 70 baada ya kupokea mpira kutoka kwa Joakim Maehle nyakati zote mbili.
Mabao yote mawili aliyafunga kwa mguu wake wa kulia.
- Mohamed Salah atuma ujumbe kwa kipa Karius
- Kipa wa Liverpool Loris Karius ashauriwa ahame
- Kipa wa Liverpool Loris Karius atishiwa maisha
Vagner Love alikombolea Besiktas bao jingine dakika ya 86 lakini hawakuwa na muda na mechi ikamalizika 4-2.
Samatta alikuwa amepiga krosi ambayo ilizalisha bao lililofungwa na Piotrowski. Aliondolewa uwanjani dakika ya 87 na nafasi yake akaingia Zinho Gano.
Sasa, nyota huyo wa Tanzania amefunga mabao matatu katika hatua ya makundi Europa League, ingawa alikuwa amefunga mengine matano mechi za muondoano za kufuzu za kabla ya hatua ya makundi.
Alifunga bao moja dhidi ya Malmo FF 20 Septemba, lakini hakufunga Sarpsborg 08 mnamo 4 Oktoba.
Katika mechi za kufuzu Europa League msimu huu, alifunga mabao mawili dhidi ya Lech Poznan, bao moja kila mechi.
Mnamo 23 Agosti 2018 Samatta, alifunga 'hat-trick' dhidi ya Brøndby IF katika Europa League kwenye mechi ambayo walishinda 5-2, na baadaye mechi ya marudiano akawafunga bao moja.
Taarifa kutoka Uingereza siku za hivi karibuni zimedokeza kwamba anatafutwa na klabu za West Ham United, Everton na Burnley kutokana na ustadi wake msimu huu katika kufunga mabao.
Samatta, mwenye kimo cha futi 5 inchi 11, amefunga mabao manane sasa Europa League msimu huu.
Masaibu ya Karius
Mjerumani huyo mwenye miaka 25 analaumiwa kwa kuwasaidia Real Madrid kushinda 3-1 kwenye fainali hiyo iliyochezewa mjini Kiev, Ukraine.Mjerumani huyo alimpa mshambuliaji wa Real Madrid Karim Benzema bao rahisi la kwanza mjini Kiev.
Baadaye, alimruhusu Gareth Bale kufunga bao la tatu la Real kutoka mbali alipojaribu kuzuia kombora lake lakini likapita mikono yake na kutumbukia wavuni.
Hilo liliwawezesha Real kushinda taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya tatu mtawalia.
Karius alitokwa na machozi baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa huku akionekana mwenye masikitiko makubwa.
Baadaye aliwaomba radhi wachezaji wenzake, wakufunzi na mashabiki.
Baadaye ilidaiwa kwamba huenda alikuwa anauguza jeraha la ubongo kutokana na mkitisiko wa ubongo.
Kabla yake kufanya kosa lililozalisha goli la kwanza, Karius aligongana na beki wa Uhispania Sergio Ramos.
Wakati wa kujiandaa kwa msimu mpya, Karius, 25, alidaiwa kusababisha bao la tatu la Borussia Dortmund katika mechi ambayo Liverpool walilazwa 3-1.
Kipa huyo alielekeza mkwaju kutoka kwa Christian Pulisic wa Dortmund kwenye njia ya Bruun Larsen aliyefunga bao lao la ushindi.
Alifanya kosa hilo siku chache baada yake kudaiwa kufanya kosa jingine mapema mwezi Julai mechi ya kirafiki dhidi ya Tranmere.
Alishindwa kudhibiti vyema mpira wa frikiki aliokuwa ameudaka na kuwawezesha wenyeji kufunga wakati wa mechi hiyo iliyomalizika kwa ushindi wa Liverpool wa 3-2 uwanjani Prenton Park.
Liverpool walikuwa wameongoza 3-0 kufikia wakati wa mapumziko kupitia mabao ya Rafael Camacho, Sheyi Ojo na Adam Lallana, kabla ya Jonny Smith na Amadou Soukouna kuwafungia Tranmere.
Kuhamia Uturuki
Loris Karius alihamia klabu ya Besiktas mwishoni mwa mwezi Agosti kwa mkopo wa miaka miwili.Alikuwa amewachezea Liverpool mechi 49 tangu ajiunge nao akitokea klabu ya Mainz ya Ujerumani mwaka 2016.
Besiktas walimaliza wakiwa wa nne katika Ligi Kuu ya Uturuki msimu uliopita, alama nne nyuma ya mabingwa Galatasaray.
Liverpool walimuuza baada ya kununua kipa Alisson kutoka Brazil na kumfanya kuwa kipa ghali zaidi duniani kwa wakati huo kwa uhamisho wa £66.8m (euro 72.5m).
Kuvuma kwa Samatta akiwa TP Mazembe
Samatta alijiunga na Genk akitokea TP Mazembe Januari 2016 ambapo alitia saini mkataba wa kumuweka katika klabu hiyo hadi msimu wa 2019/20.Amesalia na miezi 20 hivi kabla ya mkataba wake kumalizika.
Comments
Post a Comment
Here